Kikosi cha Young Africans kinatarajia kuondoka nchini leo Alhamis (Septemba 14) kuelekea Rwanda kwa ajili ya kuwafuata Al Merrikh kutoka Sudan katika mechi ya kwanza ya hatua ya kwanza ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Pele Kigali.
Mechi ya marudiano ya timu hizo itachezwa Septemba 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam na mshindi wa jumla atatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Afisa Habari wa Young Africans, Ali Kamwe, alisema anaamini mechi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu timu wanayocheza nayo ni kubwa na ina uzoefu katika michuano hiyo.
Kamwe alisema pia kila upande umejiandaa vyema kusaka matokeo chanya katika mechi ya kwanza na kujiweka kwenye mazingira bora kuelekea mchezo wa marudiano.
Alisema wachezaji wao wamejipanga kucheza katika kiwango bora katika dakika 90 za mechi ya kwanza kwa sababu wanataka kufikia malengo.
“Hatuna tatizo na Al Merrikh, tunatambua ni klabu kubwa, kongwe na huwa inafanya vizuri kwenye hii michuano, ila msimu huu inatakiwa wajipange vizuri kama sisi tulivyojipanga, dakika 90 za pale Kigali ndizo zitatupa nini kitakuja kutokea katika mechi ya marudiano jijini Dar es salaam, tunajua utakuwa mchezo mgumu sana lakini tuna imani kubwa na benchi letu la ufundi, tuna imani kubwa na wachezaji wetu.
“Pia tuna imani kubwa ya hamasa ya wanachama na mashabiki wetu ambao watasafiri kutoka Dar kwenda nchini Rwanda kwa ajili ya mechi hiyo kwa sasa hesabu ya haraka haraka ni jumla ya wachezaji 36 wamejaa, lakini kuna mashabiki ambao wapo maeneo ya mipakani ambao wanasema watasafiri asubuhi siku ya mechi na kurejea baada ya kumalizika,” alisema Kamwe.
Aliongeza amewataka wanachama na mashabiki kutokuwa na hofu na tayari wameshafanya mawasiliano kwa ajili ya wote watakaokuwa Kigali kupata nafasi ya kuingia uwanjani kushuhudia mchezo huo wa kimataifa.
“Tumezungumza na Shirikisho la Soka Rwanda, pamoja na klabu ya Al Merrikh, wameshatutumia bei za tiketi na majukwaa yake, utaratibu utakuwa mzuri kila shabiki wetu kuiona timu.” Kamwe alisema.
Naye kiungo wa timu hiyo, Maxi Nzengeli, aliyechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu mwezi uliopita amewashukuru wanayanga wote pamoja na mashabiki wa soka nchini ambao wamekuwa mchango kwa yeye kupata tuzo hiyo.
Nzengeli amesema tuzo hiyo imekuwa kama chachu ya yeye kulazimika kufanya mambo makubwa zaidi ili kuendelea kuwafurahisha mashabilki wake, pamoja na kuipatia ushindi timu yake.
“Nashukuru Mungu kwa kupata tuzo hii, nalishukuru benchi la ufundi, na wachezaji wenzangu wote, viongozi wote pamoja na mashabiki wote, inanipa moyo wa kuendelea kujituma na kufanya vizuri ili nipate tena tuzo siku zijazo,” Nzengeli alisema.
Tayari serikali kupitia Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma Mwana FA’ imesema inahitaji kuona timu hizo zinakwenda kupambana na kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Mwana FA amesema anataka kuona ushirikiano unaongezeka wakati timu hizo zinashiriki katika michuano hiyo ya kimataifa na anaamini wamefanya maandalizi mazuri.
Waziri huyo alisisitiza anataka kuona mabadiliko kwa klabu hizo mbili kuweka pembeni tofauti zao wanaposhiriki mashindano hayo ya kimataifa kwa sababu wanataka kuona timu zote mbili zinasonga mbele.