Uongozi wa Young Africans, umebainisha kuwa, timu yao itarejea ikiwa imara, huku wakihamishia nguvu kwenye mashindano mengine ikiwa ni Ligi Kuu Bara, Kombe la Azam Sports Federation na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ikumbukwe kwamba, Young Africans ni mabingwa watetezi wa ligi na kwenye anga la kimataifa michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), msimu uliopita walitolea fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika wakiwa ni washindi wa pili.
Agosti 13 walishuhudia taji la Ngao ya Jamii likielekea kwa watani wao wa jadi, Simba SC.
Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe, amesema kukwama kutwaa Ngao ya Jamii, ni sehemu ya mchezo, licha ya wachezaji wao kuonesha kiwango bora.
“Tunaamini kwamba uwezo wa wachezaji umeonekana na kila mmoja ni shuhuda namna walivyocheza kwa kujitoa. Yaliyotokea sio mwisho kwani tuna msimu mrefu na mashindano yapo mbele yetu.
“Nguvu zetu ni kwenye ligi, Kombe la Azam Sports Federation pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi tuna amini tutafanya vizuri” amesema Kamwe