Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Tanzania, Ally Mayay amelitaka Shirikisho la Soka nchini ‘TFF’ kurejesha utaratibu wa kujulisha mashabiki wa soka Tanzania juu ya kikosi cha timu ya taifa, ‘Taifa Stars’ kila kinapoitwa kambini.
Mayay amesema hayo wakati akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni nchini kuhusu kikosi cha Taifa Stars.
“Ni kweli kila kocha anakuwa na mipango yake lakini ifahamike hii ni timu ya taifa, kama inavyoelezwa ni ya watanzania na wanahabari wana haki ya kufahanu.
“Na mashabiki wengi wa Tanzania wanashangilia timu zao kama vile Simba, Young Africans, sasa linapokuja suala la taifa, mashabiki wana haki ya kupata taarifa ili waiunge mkono.
“Kama hivyo tunajiandaa kwa fainali za Mataifa ya Afrika mwakani, hivyo inapaswa tupeane taarifa ili kuwa pamoja,” amesema Mayay mchezaji wa zamani wa Stars na Young Africans
Amesema inapaswa mashabiki kuambiwa kuhusu timu yao kwani hata Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele kutoa sapoti ya fedha kwa timu za taifa.
“Naamini Shirikisho la Soka litafanyia kazi suala hilo ili kurejesha utaratibu ule ule wa kutoa taarifa mapema ili watu pia wafanye uchambuzi sababu hata uchambuzi unaofanywa na media huwa na manufaa makubwa kwa kocha,” amesema Mayay