Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Ally Mayay, amewataka viongozi wa michezo waliohitimu mafunzo ya Biashara na Masoko, watumie vizuri elimu hiyo kukuza sekta hiyo.
Mayay alitoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo hayo ya siku tano yaliyotolewa na Chuo cha Maendeleo ya Michezo cha Malya.
Mafunzo hayo yaliyoanza Jumatatu na kutamatika jana, yalifanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema washiriki waliopata mafunzo hayo wanapaswa kuhakikisha wanaendeleza sekta hiyo.
“Mnatakiwa kuwa mabalozi wakubwa katika kutoa elimu ya michezo huko mlipotoka, kwa sababu mafunzo mliyopewa nina imani yataenda kubadilisha sekta hii katika sehemu mbalimbali,” alisema Mayay
Mayay alikipongeza chuo cha Malya kwa kuendelea kutoa semina za muda mfupi na muda mrefu kwa lengo la kuongeza weledi kwa viongozi wa michezo nchini.
Mkuu wa chuo hicho, Richard Mganga, alisema wataendelea kutoa mafunzo hayo ili kuongeza taaluma kwa viongozi wa michezo nchini.
“Mafunzo haya yalikuwa na washiriki 13 kutoka mikoa mbalimbali kama Mwanza, Morogoro, Dodoma na Dar es Salaam,” alisema