Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Tanzania, Ally Mayay amesema Serikali imejiandaa vya kutosha kuhakikisha tukio la ufunguzi la African Football League (AFL) Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam linaweka rekodi.
Mayay amezungumza hayo zikiwa zimesalia takribani siku saba kabla ya ufunguzi rasmi wa ligi hiyo itakayoanza kwa Simba SC kuumana na Al Ahly ya Misri Oktoba 20, mwaka huu.
Aidha, uzinduzi wa ligi hiyo mpya kabisa Afrika inayoshirikisha timu nane utahudhuriwa na Rais wa Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino na viongozi wengine wakubwa wa soka Barani Afrika.
“Sisi tulishajipanga kwa muda mrefu, kwenye mashindano ya kimataifa achilia mbali mashindano makubwa kama AFCON lakini hata mashindano haya ya AFL ambayo yanaweka historia ya kuzinduliwa nchini, lazima kuna kitu kinapangwa kwa ajili ya kuthibitisha utayari wa serikali katika matukio makubwa kama haya.
“Kinachoendelea pale kwa Mkapa ni maandalizi ya kuhakikisha tukio hili litaweka rekodi na watu wataendelea kukumbuka kwamba Tanzania siku ya uzinduzi kilifanyika hiki na hiki sababu dunia itakuwa makini siku hiyo kuifuatilia Tanzania,” amesema Mayay.
Mbali ya Simba SC na Al Ahly ambao watacheza mechi ya marudiano Oktoba 23, mwaka huu jijini Cairo, mechi za Robo Fainali nyingine zitawakutanisha TP Mazembe dhidi ya Esperance, Enyimba dhidi ya Wydad AC na Petro du Luanda itaumana na Mamelodi Sundowns.