Rasmi Mlinda Lango chaguo la pili wa Simba SC, Ally Salim ndiye atakayekaa langoni katika mchezo wa Kariakoo Dabi dhidi ya Young Africans, ukiwa ni wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Jumapili (Novemba 05) kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Salim alidaka mechi mbili zilizopita dhidi ya Young Africans ambapo zote Simba ilishinda. Moja ya Ligi Kuu Tanzania Bara na nyingine Ngao ya Jamii.
Mmoja wa Mabosi kutoka ndani ya Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba SC, amesema kuwa Salim ndiye atakayekaa langoni katika dabi hiyo.
Bosi huyo amesema kuwa Manula ameondolewa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo, baada ya kukosa mechi fitinesi na kumuachia Salim kudaka huku Ayoub Lakred akikaa benchi.
Ameongeza kuwa, kama Manula angedaka michezo miwili ya African Football League (AFL) waliocheza dhidi ya Al Ahly ya nchini Misri, basi angeadaka dabi hiyo.
“Kama Manula angecheza michezo miwili ya AFL dhidi ya Al Ahly, basi ninaamnini angedaka dabi hiyo, sababu iliyomfanya ashindwe kukaa langoni ni yeye kukosa mechi fitinesi.
“Manula kapona kabisa na angeweza kudaka Dabi hiyo, lakini shida yeye amekosa mechi fitinesi, ataanza kudaka michezo ijayo ya ligi lakini siyo huu,” amesema Bosi huyo.
Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema: “Manula amepona kwa asilimia mia moja, lakini tatizo lake ni mechi fitinesi pekee, hivyo Salim ndiye mwenye uhakika wa kukaa golini katika dabi hii.”