Mlinda Lango wa Simba SC, Ally Salim Katoro amefunguka kuwa siri kubwa ya kuokoa Penati tatu kati ya nne zilizopigwa na Young Africans katika mchezo wa Fainali ya Ngao ya Jamii, ni maelekezo aliyopewa na Kocha wao wa makipa, Daniel Cadena.
Salim jana Jumapili (Agosti 13) alifanikiwa kuibuka shujaa kwa kuokoa Penati tatu za Young Africans zilizopigwa na Pacome Zouzoua, Yao Attohoula na Khalid Aucho na kuifanya Simba kuibuka na ushindi wa Penati 3-1.
Akizungumza baada ya kuisaidia Simba SC kuibuka na ushindi huo dhidi ya Young Africans, Salim alisema: “Kaanza namshukuru Mungu kwa ushindi huu muhimu kama timu, kwa kuwa pia ni mwanzo wa kutimiza malengo yetu ya msimu huu.
“Kuhusu siri ya mafanikio jambo kubwa ni kufuata kile ambacho Benchi la Ufundi na hususani kocha wetu wa Makipa, Daniel Cadena alichonielekeza kwa kuwa kabla ya Penati mliona aliniita na kuniambia nini natakiwa kufanya.
“Kuhusu presha kwa kuwa wachezaji wenzangu walikosa, hapana, sikuwa na wasiwasi wowote, mara nyingi nimekuwa nikifanya mazoezi ya Penati, hivyo sikuwa na hofu, bali nilijua ninawajibika kufuta makosa ya wenzangu.”