Mlinda Lango wa Simba SC Ally Salim amesema ni bahati kwake kupata nafasi ya kuitumikia kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara msimu huu na anatakiwa kuongeza umakini.
Salim amekaa langoni mwa Simba SC katika michezo kadhaa muhimu hivi karibuni kutokana na Mlinda Lango chaguo la Kwanza Aishi Manula kuwa na majeraha na kocha wa timu hiyo, Robert Oliviera ‘Robertinho’ kumtumia yeye badala ya Beno Kakolanya ambaye alikuwa chaguo la Pili.
Salim amekiri ni bahati kupata nafasi hiyo iliyokuwa adimu kwake miaka mingi, ila funzo alilopata ni kuongeza nidhamu kuanzia mazoezi kujiamini na kusikiliza zaidi maelekezo ya kocha.
“Simba ni timu kubwa yenye maono makubwa. Ukifanya vibaya unaumiza mioyo ya watu, ukifanya vizuri unaleta utulivu na amani za mashabiki.”
“Jambo kubwa zaidi nililojifunza kwenye mechi nilizocheza ni kuongeza umakini dakika zote 90, kwani kila timu inakuwa na lengo la kutikisa nyavu ili kupata hitaji lake,” amesema Mlinda Lango huyo kutoka Zanzibar
Ikumbukwe katika michezo ambayo amefanikiwa kudaka kipa huyo ni dhidi ya Ihefu, Young Africans, Namungo (Ligi Kuu Tanzania Bara), Wydad AC (Ligi ya Mabingwa Barani Afrika) na Azam FC (Kombe la Shirikisho ASFC).