Baada ya mabosi wa Simba SC kuikabidhi timu kwa makocha Seleman Matola na Daniel Cadena inadaiwa Benchi la Ufundi limewaomba kuwarejesha wachezaji waliodaiwa kusimamishwa kikosini kwani timu inakabiliwa na mechi za Ligi Kuu pamoja na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Juzi Jumanne (Novemba 07), Simba SC iliachana na Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ikiwa ni siku mbili baada ya timu hiyo kufungwa mabao 5-1 na watani zao wa jadi Young Africans kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Baada ya kuachana na kocha huyo kulikuwepo na taarifa za wachezaji sita kudaiwa kusimamishwa, lakini baadae walirejeshwa kikosini na kwenda kujumuika mazoezini na wenzao.
Wachezaji hao walifanya mazoezi ya pamoja na wenzao ikiwa ni maandalizi ya mechi ya ligi dhidi ya Namungo FC itakayochezwa leo Alhamis (Novemba 09), kwenye uwanja huo.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zinasema kuwa Matola na Cadena walifanya kikao na mabosi kuwataka wachezaji warudishwe kikosini hadi hapo baadae uamuzi mwingine utakapofanyika.
“Ukiangalia waliotakiwa kusimamishwa wote ni tegemeo kikosini. Tuna mechi ngumu mbele yetu, hivyo makocha wamewaomba viongozi wawarudishe kikosini wachezaji ili wawe na kikosi kamili kuipambania timu halafu kama kuna adhabu ni baadae.
“Leo tunacheza na Namungo FC, kuna mechi dhidi ya Asec Mimosas mwezi huu, zote tunahitaji kushinda, hivyo kama kuna matatizo kwa wachezaji hao basi viongozi wametakiwa kuyamaliza baada ya mechi hizi,” kimesema chanzo kutoka ndani ya timu hiyo.
“Pia benchi limeangalia kwamba kama (mabosi) wataruhusu wachezaji hao wakae pembeni hakutakuwepo na mbadala wao kwa sasa. Siyo rahisi, hivyo nadhani hiki kitu sasa kitafanyika Januari 2024 wakati timu ipo mapumziko na usajili wa dirisha dogo kama kuna ambao wataonekana hawafai, basi uongozi utaachana nao.”