Rais wa Guinea anayemaliza muda wake Alpha Condé atawania muhula wa tatu katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Oktoba 18, mwaka huu.
Hayo yanajiri wakati nia ya Alpha Condé ya kuwania katika uchaguzi wa urais nchini Guinea ilizusha maandamo makubwa kwa miezi kadhaa na kusababisha watu kuuawa mwaka 2019.
Tofauti na chaguzi mbili za urais zilizopita ambapo Alpha Condé mwenyewe alitangaza kugombea, hivi sasa chama chake cha RPG, na vyama vingine vinavyomuunga mkono ndivyo vimemuomba kuwania kwenye kiti cha urais katika uchaguzi ujao.
Katika mkutano mkuu wa chama chake uliokutana Agosti 5 na 6, wajumbe wote waliafikiana kwamba hakuna mtu mwingine ambaye anaweza kupelekea ushindi wa chama chao isipokuwa rais Condé.
Kwa kujibu ombi hilo, Alpha Condé ameweka masharti: “ikiwa mnataka nikubali pendekezo lenu, inabidi mkubali kuwa RPG, chama chetu, kinatakiwa kurudi kuwa kama kile kilichokuwa hapo awali, chama kisichombagua yeyote. ” amesema konde.