Kundi la kigaidi la Al-Shabaab lenye makazi yake nchini Somalia limetangaza kutekeleza shambulizi katika kambi ya Kulbiyow ya kikosi cha Kenya, iliyo karibu na mpaka wa nchi hizo mbili.

Msemaji wa kundi hilo, Sheikh Abdiasis Abu Musab ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa kundi hilo lilifanikiwa kutekeleza shambulizi hilo kwa kutumia magari yenye mabomu.

“Wapiganaji wetu wawili walivurumisha magari yaliyokuwa na mabomu na kuyalipua kwenye lango la kambi hiyo ya mji wa Kulbiyow kabla ya wapiganaji wengine kuingia. Baada ya makabiliano makali, tumefanikiwa kuiteka kambi,” msemaji huyo wa Alshabaab anakaririwa

Aidha, amedai kuwa kundi hilo liliwaua wanajeshi zaidi ya 50 na kupora magari pamoja na silaha. Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Kenya, Kanali Paul Njuguna amekanusha taarifa za kuporwa kwa silaha na magari.

Msemaji huyo wa Kenya amedai kuwa taarifa hizo ni za uongo na kwamba kikosi cha Kenya kinaendelea na oparesheni chini ya kikosi cha umoja wa Afrika.

“Ni uongo. Operesheni ya kijeshi inaendelea. Tunaendelea kupokea taarifa,” alisema Kanal Njuguna.

Kikosi cha Umoja wa Afrika kiko nchini Somalia kikiunga mkono Serikali halali ya nchi hiyo kupambana na kundi hilo lililoungana na kundi hatari la Al-Qaeda.

Video: RC Zelote awacharukia Wakurugenzi kuhusu TASAF
FA Cup Kuendelea Wikiendi Hii