Bondi wa Uingereza, Amir Khan usiku wa leo atakuwa na kibarua kizito atakapopanda ulingoni kuzichapa na Samuel Vargas ikiwa ni jaribio lake la pili la kufuta kumbukumbu mbaya.

Khan ambaye aliwahi kuwa bingwa wa dunia wa masumbwi, anatakiwa kuifuta kumbukumbu mbaya ya kuzimishwa na Canelo Alvarez kwenye pambano lao lililomuachia makovu makubwa kwenye fuvu la kichwa chake na kufifisha ndoto yake ya kuzichapa na Manny Pacquiao au Floyd Mayweather.

Bondia huyo ameeleza kuwa hivi sasa yuko katika hali nzuri kwa namna zote na kwamba ana uhakika atashinda pambano hilo na kupata nafasi ya kupanda ulingoni dhidi ya Manny Pacquiao ambaye hivi sasa ndiye bondia anayezungumziwa zaidi akiwa hajamtaja mpinzani wake.

“Ni kuhusu kuweka heshima, kupigana na majina ambayo mashabiki wangependa. Pambano langu na Manny Pacquiao litakuwa kubwa kwa sababu yeye ni gwiji. Na hayo ndiyo mapambano ambayo natakiwa kushinda,” alisema Khan.

Kuhusu kukosolewa kuwa umri wake ni mkubwa, amedai kuwa hivi sasa ana miaka 31 na anaona hata akichana na masumbwi hana cha kufanya na bado ana uwezo.

Aliwatolea mfano Manny Pacquiao ambaye ana umri wa miaka 38 na bado anapigana pamoja na Floyd Mayweather aliyestaafu akiwa na umri wa miaka 40.

Hata hivyo, Vargas amemuonya Khan kuwa asijaribu kumchukulia poa leo usiku na kwamba anaweza kumzimisha kwa ngumi moja.

“Ninatakiwa kumpiga ngumi moja tu. Kila mmoja anajua kuwa Khan ana taya laini. Kila mtu amekuwa akimzungumzia kuhusu kasi yake ya kurusha masumbwi, lakini hiyo ilikuwa zamani. Mimi nina uwezo wa kumzimisha mapema,” alisema Vargas.

Khan na Vargas wanapambana katika uzito wa Welterweight wa kilo 67.

Video: Mkuu wa Wilaya ya Busega awataka wananchi kujitokeza kwenye ziara ya JPM
Video: Jerry Muro aichana hotuba aliyoandaliwa, asema ni upuuzi