Beki wa zamani wa Klabu za Simba SC na Young Africans Amir Maftah, amewataka Mashabiki wa Soka Tanzania kumpa muda kiungo Ismail Sawadogo, ili kuona anafaa kufananishwa na Patrick Mutessa Mafisango.
Maftah ametoa kauli hiyo kufuatia sifa anazopewa Sawadogo aliyesajiliwa Simba SC wakati wa Usajili wa Dirisha Dogo mwezi huu (Januari), huku akicheza mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC.
Maftah amesema kiungo huyo kutoka Burkina Faso mchezaji mzuri ila bado ni mapema kuona kama atafanana kiuchezaji na Mafisango moja kwa moja.
“Nilitazama ile mechi bado kwa sasa ni ngumu kumfananisha moja kwa moja na Mafisango ingawa kwa muda mchache ameonyesha ana kitu mguuni kwake ngoja tumpe muda kidogo.”
“Kwa upande wa Mafisango yeye ulikuwa unamuona wakati wa kuzuia, katikati ya uwanja, alikuwa akienda kufunga, anakaba na anatengeneza nafasi huyu Sawadogo kuna baadhi ya vitu anendana naye japo vingine sijaona akivitumia sawa sawa,” amesema Maftah
Kabla ya kutua Simba SC Sawadogo alikua anaitumikia Difaâ El Jadida ya Morocco, iliyomsajili kutoka Enppi SC ya Misri.
Wengine waliosajiliwa Simba SC kupitia Dirisha Dogo ni Saido Ntibazonkiza (Burundi), Jean Baleke (DR Congo) na Mohamed Mussa (Zanzibar).