Mkuu wa Mkoa wa Dar esa Salaam Amos Makalla amewahimiza Mashabiki wa soka mkoani humo na sehemu za karibu, kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumapili (Machi 13), kushuhudia mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Simba SC dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Kiongozi huyo amesema anafahamu mchezo huo utakuwa na ushindani lakini anaamini Simba SC itaendelea kufanya vizuri kwenye Uwanja wake wa nyumbani, hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi bila kusahau kuzingatia sheria za mamlaka ya afya kuhusiana na kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19.
Makalla amesema anaamini Simba SC itafanya vizuri katika mchezo huo na kuendelea kujiweka kwenye mazingira bora ya kusonga mbele katika michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Makala amesema: “Tumepata fursa ya mashabiki kushuhudia mchezo huo, bila kujali itikadi ya timu zetu pendwa, tujitokeze uwanjani kuisapoti Simba SC kwa sababu ni timu pekee iliyopo kwenye ramani ya michezo ya kimataifa kwa hapa Tanzania,”
Simba SC ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane katika mchezo wa Mzunguuko wa tatu wa Kundi D, Februari 27 mjini Berkane-Morocco hivyo itahitaji kulipa kisasi kwa kusaka ushindi ili kurejea kileleni mwa msimamo wa Kundi hilo.
Kabla ya mchezo huo Simba SC ilikua inaongoza msimamo wa Kundi D kwa kuwa na alama 04, huku Berkane iliyopoteza mchezo wa Mzunguuko wa pili dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast ilikua na alama 03.
Hadi sasa Msimamo wa Kundi D, unaonyesha kuwa RS Berkane inaongoza ikiwa na alama 06, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama o4 sawa na USGN ya Niger huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiburuza mkia ikiwa na alama 03.