Kijana wa aliyekua katibu mkuu wa shirikisho la soka barani Afrika CAF Amr Fahmy ametangazwa kuwa katibu mkuu wa shirikisho hilo.
Amr mwenye umri wa miaka 34, ni mtoto wa Mostafa Fahmy ambaye alilitumikia shirikisho la soka barani Afrika CAF kwa miaka 28 kama katibu mkuu.
Amr ambaye ni raia wa Misri, anachukua nafasi ya Hicham El Amrani wa Morocco ambaye alikaa kwenye nafasi hiyo tangu Oktoba mwaka 2010 hadi Machi 2017 alipotangaza kujiuzulu bila sababu.
Fahmy alipendekezwa na Rais wa CAF Ahmad kwenye Kamati ya Utendaji, kisha jina lake lilipitishwa katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika jana mjini Rabat, Morocco.
Anthony Baffoe (Kulia), Amr Fahmy (katikati) na Essadik Alaoui (Kushoto)
Makatibu wawili wasaidizi pia wameteuliwa kwa vigezo vile vile, wa kwanza ni Mghana Anthony Baffoe ambaye anakuwa Msaidizi upande wa Maendeleo na Mashindano na wa pili ni Mmorocco, Essadik Alaoui anayekuwa Msaidizi upande wa Utawala na Fedha.