Mchezaji wa zamani wa klabu za Kagera Sugar, Simba SC na Young Africans Amri Kiemba amejitosa kwenye sakata la kufanya vibaya kwa Azam FC katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Azam FC imeshapoteza michezo mitatu, imeshinda mara mbili na kuambulia sare mara moja msimu huu 2021-22.
Jumapili (Novemba 21) Azam FC ilipoteza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC FC kwa kufungwa mabao 2-1, Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Kiemba ambaye ni mchambuzi wa Michezo wa Radio Clouds FM ametoa andiko ambalo kwa ufahamu wake anaamini ndio chanzo cha kukwama kwa Azam FC msimu huu.
Kiemba ameandika: Azam tangu imewasimamisha Aggrey Morris, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Mudathir Yahya, nafikiri kuna mahali hapako sawa.
Ukiona wachezaji waandamizi wanasimamishwa ujue kwenye uongozi, benchi la ufundi au wachezaji kuna mahali hapako sawa!
Kupata matokeo kwa sehemu ambayo iko hivyo ni ngumu kwa sababu, hao wachezaji waandamizi waliosimamishwa tayari kuna wachezaji wengine walikuwa wanaamini ndio walikuwa wanawapambania kwenye mambo yao mengi. Kusimamishwa kwao kuna wachezaji wanahisi ni kunyimwa haki zao na kuzungumza.
Ni kama wamekata ‘link’ ya watu ambao wanaweza kuukabili uongozi, na waliosimamishwa unakuta ndio walikuwa wanategemewa na wachezaji wengine kuzungumza kwa niaba yao. Na mambo mengine yalikuwa yanafanyika baada ya hao wachache kujitoa mhanga.
Kwa hiyo unakuta sasa hivi hata mwalimu anapata wakati mgumu kufanya kazi. Kama wachezaji waliopo wanahisi haikutendeka haki wakati wenzao wanasimamishwa ni ngumu kufanya kazi na kupata matokeo.
Inawezekana uongozi wa Azam namna ulivyokabiliana na tatizo lililokuwa linaendelea ndani mpaka kupelekea kuwasimamisha wachezaji, huenda imeathiri timu.
Ukiangalia namna Azam inavyocheza na namna ambavyo walijiandaa kwa msimu huu huoni kama wanafanikiwa.