Mwanaume mmoja aliyetajwa kwa jina la Chinindu Innocent, mkaazi wa jimbo la Abia nchini Nigeria anashikiliwa na jeshi la polisi kwa kosa la kumteka mama wa aliyekuwa mpenzi wake.
Innocent anashikiliwa pamoja na wenzake watatu waliohusika kwenye tukio la utekaji huo, siku chache baada ya kupewa kiasi cha N300,000 kisha kumuachia mateka wao.
Kwa mujibu wa maelezo ya mahojiano kati ya Innocent na jeshi la polisi, yaliyochapishwa na PUNCH, Innocent alieleza kuwa alichukizwa na kitendo cha usaliti ambacho alifanyiwa na mpenzi wake na kisha akaamua kwenda kumueleza mama yake [mama wa binti] ambaye walikuwa wanafahamiana kwani alikuwa akitembelea nyumba hiyo.
“Kwanza nilipogundua nilizungumza na mtoto wake lakini mtoto wake alitishia kuua uhusiano wetu. Kwakuwa nampenda sana nikaenda kumueleza mama yake, lakini naye hakufanya kitu chochote, nikakasirika nikaamua kupanga namna ya kuwaadhibu,” Innocent anakaririwa.
Alisema kuwa alizungumza na binamu yake aliyemtaja kwa jina la Aparazu Ogwu ambaye walifikia muafaka kuwa wamteke mama wa mpenzi wake, pamoja na mambo mengine wakilenga kupata fedha nyingi kama sharti la kumuachia. Baada ya kukubaliana waliwatafuta watu wengine watatu ambao ni genge la wahalifu ili wawasaidie.
“Tulikubaliana wakati wa utekaji huo na mimi niwe nyumbani kwao. Kwahiyo walituteka wote na mimi nikiwemo wakatupeleka kwenye msitu wa kijiji cha Omuma. Lile genge tulilolikodi lilihitaji kupewa N1.5 milioni ili watuachie, lakini waliishia kupata N300,000 tu,” alisema.
Innocent alidai kuwa mgao huo mdogo uliwafanya watekaji hao kuchukua kiasi chote cha fedha bila kuwapa mgao hata kidogo yeye na binamu yake, kinyume na makubaliano.
“Walikataa kutupa kiasi chochote, walisema kuwa wanapowateka watu huwa wanapewa fedha nyingi lakini sasa hivi wamepewa fedha kidogo ambazo haziwatoshi,” alisema.
PUNCH imeeleza kuwa wakati pande hizo zinafanya mawasiliano, Polisi walikuwa wakiwafuatilia na ndipo walipowakamata wakiwa kwenye mchakato wa kudaiana.