Mwanamke aliyetajwa kwa jina la Onyinyechi Osoneye, amejikuta mikononi mwa vyombo vya dola mwishoni mwa wiki iliyopita kwa tuhuma za kumuuza mtoto wake siku moja baada ya kujifungua salama.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na maafisa wa polisi nchini Nigeria, mwanamke huyo alifanya biashara ya kumuuza mwanae wa kiume kwa familia ya Bwana na Bibi John Chukwu, waishio jijini Lagos kwa kiasi cha N250,000.
Jeshi la Polisi la Lagos limeeleza kuwa katika mahojiano, Onyinyechi alikiri kumuuza mwanae huyo na kwamba alisaidiana na mama yake mzazi ambaye pia alimsaidia awali kuficha ujauzito ili baba yake asiufahamu. Mwanamke huyo alisema kuwa waliamua kushirikiana na mama yake katika mpango huo kwakuwa baba yake ni mkali na asingekubali kumuona amepata ujauzito bila ndoa.
Uchunguzi ulibaini kuwa Onyinyechi alifika katika hospitali ya Ikota jijini humo na kufanikiwa kumpata mtoto wa kiume, Machi Mosi mwaka huu. Hata hivyo, mtoto huyo aliondolewa ghafla hospitalini hapo na kuhamishiwa katika hospitali nyingine inayofahamika kwa jina la Orile.
Kwa mujibu wa maelezo ya watuhumiwa yaliyowekwa wazi na jeshi la polisi, mtuhumiwa mmoja aliyetajwa kwa jina la Prisca Okocha alikiri kuwa yeye ndiye aliyekuwa mtu wa kati katika biashara hiyo haramu na kwamba alifanikisha kumuuza mtoto huyo kwa N850,000 lakini alimlipa mama wa mtoto N250,000.