Mlinda mlango kutoka Cameroon na klabu ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi Andre Onana, amesema anatamani kuhamia katika ligi ya England, ili kutimiza ndoto zake.
Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 23, aliyasema hayo mara baada ya mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Chelsea, uliomalizika kwa sare ya mabao manne kwa manne, usiku wa kuamkia leo Jumatano.
Licha ya kusaini mkataba wa muda mrefu wa kuendelea kuitumikia Ajax Amsterdam, Onana amedhihirisha suala hilo mbele ya waandishi wa habari ambao walitaka kufahamu nini malengo yake, baada ya kuendelea kuonyesha uwezo mkubwa anapokua langoni.
Mkataba mpya wa Onana na klabu ya Ajax Amsterdam, unatarajiwa kufikia kikomo mwezi Juni mwaka 2022.
“Hapa England kuna soka la ushindani, kila mchezaji anatamani kucheza katika ligi ya nchi hii, ninatumai ipo siku ndoto zangu za kuja hapa, zitatimia”
“Ligi ya England imekua na mvuto wa aina yake, kila wiki nimekua naifuatilia. Ninaamini hakuna litakaloshindikana kwa mimi kuwa hapa katika siku za maisha yangu ya kucheza soka, kwa sasa ninaendelea kuheshimu mkataba wangu na Ajax, ninafurahia maisha nikiwa na klabu yangu tangu nilipokua chaguo la kwanza.” Alisema Onana.
Onana amekua akifuatiliwa kwa ukaribu na baadhi ya klabu za barani Ulaya, huku vyombo vya habari vya England vikizitaja Tottenham Hotspur na Manchester United kuwa katika mawindo makali ya kuisaka saini yake.
Onana alijiunga na Ajax Amsterdam mwaka 2015 akitokea FC Barcelona, baada ya kukuzwa kwenye kituo cha La Masia.
-
Ndayiragije ataja jeshi litakaloivaa Equatorial Guinea, Libya
-
Kwa shilingi 3000 na 5000 utashuhudia Taifa Stars Vs Equatorial Guinea
Msimu uliopita aliisaidia Ajax Amsterdam kufika hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, tangu mwaka 1997, na alikuwa sehemu ya kikosi cha Cameroon kilichoshiriki fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2019) zilizounguruma nchini Misri.