Mlinda Lango kutoka nchini Cameroon Andre Onana amekubali kukosolewa na mashabiki baada ya kuruhusu bao lake la kwanza Old Trafford kwenye mchezo wa mwisho wa kujiandaa na msimu dhidi ya Lens.
Hata hivyo, Manchester United ikaibuka na ushindi wa mabao 3-1 lakini kipa huyo alipondwa baada ya kushindwa kuzuia mpira wa mbali uliopigwa na mchezaji wa Lens, Florian Sotoca na kuingia moja kwa moja kwenye nyavu.
Baada ya mchezo huo kumalizika Onana alisema ataubeba mzigo wa lawama kichwani kwani ndio sehemu ya kujifunza kwa hiyo hatajali maneno ya mashabiki mitandaoni.
“Nitawajibika kwa kila kitu hususan mabao tunayoruhusu. Ninajivunia walichofanya mabeki wangu. Mimi ndiye kila kitu nimepokea maneno ya mashabiki walionikosoa. Tunaweza kucheza kwa kiwango bora lakini tunapaswa kurekebisha makosa pia,” alisema kipa huyo aliyesajiliwa kwa Pauni 47 Milioni.
Erik Ten Hag alianzisha kikosi cha nguvu kilichosheheni mastaa dhidi ya Lens kutoka Ufaransa huku mfungaji wao bora Marcus Rashford akianza kwenye safu ya ushambuliaji na Mason Mount akicheza mechi yake ya kwanza ndani ya Uwanja wa Old Trafford.
Aidha kwa upande wa Mount pia alipondwa na mashabiki baada ya kukosa bao la wazi kipindi cha kwanza kutokana na pasi nzuri aliyowekewa na Alejandro Garnacho.
Shabiki mmoja aliandika kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter: Tulitumia pesa nyingi kumsajili Mount lakini kumbe hakuna kitu.”
Mwingine akaandika: “Sikushawishika kabisa na usajili wa Mount.”
Mwingine alimlaumu Ten Hag sababu ya kumsajili Mount: “Kwa nini Ten Hag alimsajili Mount sielewi kabisa.”
Kabla ya mechi hiyo mashabiki walimkaribisha mchezaji wao mpya Rasmus Hojlund ambaye alisajiliwa kwa United kwa ada ya Pauni 72 Milioni kutoka Atalanta inayoshiriki Serie A.