Klabu ya Chelsea imeendelea kuitahadharisha Inter Milan kwa kuutaka uongozi wa klabu hiyo ya mjini Milan-Italia, kuhakikisha wanafikia dau la Pauni milioni 40, ili kukamilisha usajili wa Mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji Romelu Lukaku.
Kwa mujibu wa Mtandao wa 90min, klabu hizo mbili zimekuwa kwenye mazungumzo ya usajili wa Lukaku kwa miezi kadhaa, huku Chelsea wakikataa ofa kadhaa kutoka kwa Inter Milan na pia wakitafuta kurejesha fedha nyingi iwezekanavyo kutoka kwa uwekezaji wao wa awali wa pauni milioni 97.5 walipomnunua.
Jaribio la Inter kutaka kumsajili tena Lukaku kwa mkopo lilizuiwa haraka na Chelsea, ambao wanataka sasa auzwe jumla.
Ofa ya takriban Pauni milioni 30 imekataliwa hivi majuzi na Chelsea, huku vyanzo vikithibitisha kwamba “The Blues’ hao wanashinikiza Inter kuongeza dau lao kwa pauni milioni 10 nyingine.
Inter Milan hawana bajeti kubwa ya uhamisho na kwa hiyo wana nia ya kuepuka kutumia fedha nyingi kwa Lukaku, ingawa kuuzwa kwa Mlinda Lango Andre Onana kwenda Manchester United kunaweza kuwapa ‘The Nerazzurri’ nafasi ya kuongeza dau.
Ili kujaribu na kusaidia hatua hiyo, Lukaku yuko tayari kukatwa mshahara mkubwa. Analenga tu kurejea Inter msimu huu wa majira ya joto licha ya kuvutia nia kutoka mahali pengine.
Juventus wameulizia kuhusu Lukaku baada ya Chelsea kuonesha nia ya kutaka kumnunua mshambuliaji wa ‘Bianconeri’ hao, Dusan Vlahovic moja ya majina mengi kwenye orodha fupi ya wachezaji wanaolengwa na The Blues lakini Lukaku hataki kujiunga na timu nyingine ya Serie A.
Lukaku pia amepoteza nafasi ya kuhamia Saudi Arabia, ambayo ilifanya juhudi mpya kumshawishi mshambuliaji huyo kuelekea Mashariki ya Kati baada ya kuwasili mapema msimu huu wa majira ya joto.
Ofa yao imesalia mezani, lakini Lukaku hataki kukubali huku akisubiri Inter wafikie makubaliano.