Mlinda Lango wa Man Utd Andre Onana amekiri kufanya makosa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich.
Man Utd walipoteza mchezo huo kwa kukubali kufungwa 4-2, wakiwa ugenini mjini Munich, huku Mlinda Lango huo kutoka nchini Cameroon akitupiwa lawama kwa kiwango duni alichokionesha.
Onana aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea Inter Milan alifanya makosa yaliyopelekea wapinzani wao kupata bao la kuongoza kupitia kwa Reloy Sane, na alipohojiwa kuhusu kosa hilo alikiri kufanya kosa.
Mlinda Lango huyo alipohojiwa mara baada ya mchezo huo alisema: “Baada ya mimi kukosea, tulishindwa kuuhimili mchezo na mimi ndiye niliyeiangusha timu”
“Ni kosa langu, lazima nijifunze kutokana na hili kosa kuanzia sasa na siku zijazo.”
“Nina kazi ya kuhakikisha nathibitisha ubora wangu kwa sababu kusema ukweli mwanzo wangu Manchester United sio mzuri.”
Huo unakuwa mchezo wapili mfululizo kwa Man Utd kupoteza kwa siku tano zilizopita, kwani kabla ya kuelekea mjini Munich, Ujerumani timu hiyo ilikubali kichapo cha 3-1 kutoka kwa Brighton.