Mshambuliaji wa kutoka nchini England na klabu ya West Ham Utd, Andy Carroll huenda akakaa nje kwa muda wa wiki sita baada ya kuumia misuli ya paja mwanzoni mwa juma hili.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, alilazimika kutolewa uwanjani wakati wa mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England ambapo Wet Ham Utd walipambana na Bournemouth, na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Hii inakua kama mkosi kwa Carroll, kutokana na kupata majeraha ya mara kwa mara ambapo kama itakumbukwa vyema aliwahi kuwa nje ya uwanja wa kipindi kirefu, kabla ya kurejea mwezi Septemba mwaka 2015.

Kurejea kwake ilionekana kama faraja Kwa West Ham Utd, kutokana na juhudi kubwa ambazo alizionyesha na alifanikiwa kufunga mabao muhimu katika baadhi ya michezo aliyocheza msimu huu.

Kabla ya hapo, alikuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi saba, kufuatia upasuaji wa goti aliofanyiwa.

“Mambo yakienda tunavyotarajia, basi atatusaidia katika sehemu ya mwisho ya michezo itakayotukabili mwishoni mwa msimu huu,” amesema meneja wa West Ham Slaven Bilic alipokua akithibitisha taarifa za kukaa nje kwa mshambuliaji huyo.

Carroll, ambaye aliwahi kuitumikia klabu ya Newcastle Utd, alijiunga na West Ham Utd akitokea Anfield yalipo makao makuu ya klabu ya Liverpool kwa ada ya uhamisho wa paund million 15 mwezi Juni mwaka 2013.

Kwenye msimamo wa ligi msimu huu ambao bado unaendelea, West Ham Utd wapo kwenye tano bora, na kama wataendelea kufanya vyema huenda wakafanikiwa kucheza michuano ya barani Ulaya msimu wa 2016-17.

Rwanda Ipo Tayari Kwa CHAN 2016
Lowassa ashauri njia ya kupata maridhiano Zanzibar, alaani Ubaguzi