Kiungo Mshambuliaji ‘WINGA’ wa Argentina, Ángel Di María amesema michuano ya Copa America 2024 itakuwa mashindano yake ya mwisho akiwa na Albiceleste, akihitimisha mbio za miaka 16 ya kuitumikia timu ya taifa.
“Nitaondoka kwenye Timu ya Taifa ya Argentina baada ya Copa America. Imekwisha kwangu, itakuwa michuano ya mwisho,” alisema mshindi huyo wa Kombe la Dunia akiiambia redio ya Argentina Urbana Play 104.3.
Di Maria, ambaye hayumo katika kikosi cha Argentina kwa ajili ya mechi za kufuzu za CONMEBOL wiki hii kutokana majeraha, alisema moja ya sababu za kurejea Benfica, timu ambayo ilimntambulisha Ulaya mwaka 2007 akitokea Juventus ilikuwa kumsaidia kufikia Copa America mwakani katika hali nzuri.
“Nilikuja Benfica chaguzi zangu za kuendelea katika timu ya taifa,” aliongeza Di Maria.
“Nilijua ni lazima nicheze katika timu nzuri ili niwe katika kiwango kizuri. Nataka kucheza Copa America ijayo na ninafanya kila niwezalo kuwa bora katika klabu yangu na kila ninapoichezea Argentina.”
Michuano ya Copa America 2024 itafanyika kati ya Juni 20 na Julai 14, mwakani nchini Marekani.
Di Maria alikuwa shujaa kwa nchi yake baada ya kufunga mabao katika fainali mbili ambazo Argentina ilishinda mataji katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Alifunga bao pekee dhidi ya Brazil katika fainali ya Copa America mwaka 2021 na la kwanza kwa timu yake katika ushindi dhidi ya Ufaransa kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2022.
“Nilisema mara nyingi kwa familia yangu, Copa America ilibadilisha maisha yetu milele,” alisema Di María.
“Kwa sababu ilikuwa mara zote kufika huko kwenye fainali na kushindwa, hadi siku niliporudi nyumbani na waliniambia wakati huu umeshinda.
“Baada ya kuwa bingwa wa dunia, watu wanakutambua kila mahali. Ninapeleka binti zangu shuleni nchini Ureno na kuna watoto ambao wana umri wa miaka mitano au sita na wananiambia: “Wewe ni bingwa wa dunia. Hilo ndilo jambo pekee wanalojua kunihusu.”
Di Maria, ambaye aliwahi kuzichezea Paris Saint-Germain, Manchester United na Real Madrid katika maisha yake ya soka barani Ulaya, ameifungia Argentina mabao 29.
Mbali na mataji ya Kombe la Dunia na Copa America, alishinda medali ya dhahabu huko Beijing 2008 akiwa na Argentina na Kombe la Dunia la FIFA U-20 mnamo 2007.