Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini TFF Angetile Osiah ameshangazwa na kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Biashara United Mara Seleman Mataso, kufuatia sakata la mvutano wa Mdhamini Mwenza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mvutano huo uliibuka kufuatia Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC kugomea kuweka nembo ya kampuni ya GSM, iliyoingia mkataba wa zaidi ya Shilingi Bilioni 2 na Shirikisho la Soka nchini TFF mapema mwezi Novemba.

Angetile ameshangazwa na kauli ya Mataso ambaye alinukuliwa akisema anachojali ni fedha, na klabu yake haitahusika na mambo ya mvutano yaliyoshika hatamu kwa majuma mawili kabla ya mchezo wa Jumamosi kati ya Simba SC dhidi ya Young Africans.

Angetile amesema: “Nimeshangaa kusoma kwamba eti kiongozi wa klabu ya Biashara anasema anachojali “ni fedha, na hayo mambo mengine hayawahusu”. Hicho ni kiwango kikubwa cha kutojua wajibu wake kama kiongozi wa klabu ya Ligi Kuu, haki za klabu hiyo na vyanzo vya mapato”

“Kwa kiongozi kama huyo unaona dhahiri ni kwa sababu gani Biashara ilishindwa kwenda Libya kucheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho baada ya kushinda 2-0 nyumbani. Na unaona dhahiri sababu za timu hiyo kwenda kwa mbinde Djibout kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho”

“Hawa si aina ya viongozi wanaotakiwa kuongoza klabu za Ligi Kuu kama upeo wake wa masuala ya udhamini, uwazi na haki za klabu ni mdogo kiasi hicho. Lakini ni muhimu pia kwa Bodi ya Ligi kuanza kukuza chapa ya Ligi Kuu kama bidhaa yake kubwa badala ya kung’ang’ania mfumo wa zamani wa udhamini”

“Haiwezekani Ligi Kuu ikawa na wadhamini wakuu wawili, mmoja akiwa amedandia gari wakati safari imeshaanza. Ni kituko kingine hicho.”

Hata hivyo Simba SC haikuweka nembo ya Mdhamini Mwenza kwenye jezi zake, huku agizo lao la kutaka mambongo ya Mdhamini huyo kuondolewa likitekelezwa kwenye mchezo wao dhidi ya Young Africans uliomalizika kwa sare ya 0-0.

Simba SC waitikia ombi la Mwekezaji
Dewji kuchangia Bilion 2 ujenzi Mo Simba Arena