Mjumbe wa Bodi mpya ya Tanzania Girl Guides Association (TGGA), Anna Abdalah, amewataka viongozi Wanawake kukutana na Wasichana kuwapiga msasa wa kuwaandaa kuwa viongozi bora wa baadaye.
Anna Abdalah ambaye amekuwa kiongozi wa muda mrefu nchini, ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya TGGA, Mikocheni Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa ana mpango wa kuwaalika viongozi mbalimbali Wanawake akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akutane na Wasichana wanachama wa TGGA wawafundishe maadili ya uongozi kwa lengo la kuwaandaa kuwa viongozi bora wa baadaye.
“Nataka siku za usoni,tuwaalike viongozi mbalimbali akiwemo, Samia Suluhu Hassan, Naibu Spika wa Bunge, Wabunge na Mawaziri Wanawake ili mje mjumuike nao pamoja, mjifunze mambo mbalimbali ya uongozi na mhamasike, ili siku moja nanyi mje kuwa kama, Samia, Kamishna, Spika wa Bunge, Wabunge na hata uwaziri pia” alisema Anna Abdalah, huku akipigia makofi na waalikwa katika hafla hiyo.
Katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Engera Kileo, ilihudhuriwa na wanachama wa chama hicho, wakiwemo pia wasichana watatu waliotoka Rwanda, Uganda na Madagasca waliokuwepo
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TGGA, Symphorosa Hangi, amewataja Wajumbe wa Bodi hiyo kuwa ni; Zakia Meghji, Anna Abdalah, Grace Makenya, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema na Mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Tunu Pinda. Mwenyekiti wa Bodi hiyo atateuliwa miongoni mwao.