Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda leo Januari 28, 2020 amepata nafasi ya kuzungumza na wabunge ambapo amesema kuwa tofauti za itikadi zisiwagawe wabunge na wananchi kwani wote ni watanzania.
Akizungumza leo katika kikao cha kwanza cha mkutano wa Bunge wa 18 ambapo maspika wastaafu walikuwa wakikabidhiwa majoho na Spika wa sasa Job Ndugai, amesema kuwa mfumo wa vyama vingi ulianzishwa na wabunge wenyewe hivyo ni sheria kuwa na vyama vingi na havimaanishi kugawa nchi.
”Na sisi kama tukitaka kujenga nchi hii uzalendo lazima kiwe kitu cha kwanza kwa sababu nchi hii ni ya kwetu sisi wote, tofauti zetu za itikadi zisitugawe sisi ni watanzania hata kuwe na vyama vingi, kama tunavyosema ilianzishwa na bunge hili, ni sheria sio kwamba ni hiari ni sheria kuwa na vyama vingi ni sheria tulipitisha sisi wenyewe hapa” Anne Makinda.
Pia amesisitiza juu ya unyenyekevu ambao wabunge wanatakiwa kuwa nao kwa wananchi wao ambao wanautumia kama daraja kufikisha shida zao ili ziweze kutatuliwa, hivyo amewaomba waendelee kuwa wanyenyekevu ili wananchi wawe huru kufikisha shida zao kwao.
Ameongezea kuwa mbunge yeyote ambaye siyo mnyenyekevu kwa wananchi wake ni mbunge mwenye mashaka.
Aidha amewaasa wabunge kuendelea kujifunza kila siku kwa wazee waliowatangulia na amewataka kuwa wazalendo kila siku kwa ajili ya nchi yao.