Promota wa mwanamasumbwi, Anthony Joshua, Eddie Hearn amethibitisha kuwa Pambano la marudiano kati ya Andy Ruiz Jr na Anthony Joshua linatarajiwa kufanyika mwezi Disemba mwaka huu nchini Saudi Arabia.

Kumekuwa na tetesi kuwa Ruiz Jr hayupo tayari kwa pambano hilo, lakini Hearn amesema kuwa mabondia wote wawili wamesaini kucheza pambano hilo linalotarajiwa kufanyika Disemba 7 mwaka huu.

Ruiz aliushangaza ulimwengu wa masumbwi kwa kumchakaza Joshua mwezi Juni mwaka huu na kutawazwa kuwa bingwa wa dunia.

Aidha, bingwa huyo mpaka sasa hajawaarifu chochote mashabiki wake kupitia mitandao ya kijamii kuhusiana na pambano hilo la marudiano tangu lilipotangazwa siku ya Ijumaa iliyopita.

Katika mkutano na wanahabari, ambao hata hivyo si Joshua wala Ruiz ambaye alihudhuria, promota Hearn alitangaza kuwa mpambano huo utafanyika katika uwanja wa wazi katika kitongozji cha Diriyah, nje kidogo ya jiji la Riyadh nchini Saudi Arabia.

”Mabondia wote wawili wameshatia saini ya pambano hilo, vyombo vya usimamizi wa ngumi tayari vimeshaarifiwa,” amesisitiza Hearn.

Hata hivyo, Ruiz alimpoka Joshua mikanda ya IBF, WBA na WBO Juni mosi mwaka huu baada ya kumuangusha mara nne kabla ya mpambano huo kukatishwa na mwamuzi.

 

 

Video: Kesi Lissu, Ndugai kuunguruma Kisutu, Ripoti ajali Moro yatesa viongozi
Lugha ya kiswahili yapendekezwa kuwa lugha ya nne SADC