Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Antoine Griezmann amekiri anafuatilia ushujaa wa ajabu wa Lionel Messi kule Inter Miami, huku akisema bado ana matumaini ya kumalizia soka lake kwa kucheza Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
Messi mwenye Umri wa miaka 36, amefunga katika mechi zake zote za Inter Miami hadi sasa akiwa amefunga mabao tisa kwenye mechi sita, ikiwa ni pamoja na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Philadelphia Union juzi Jumanne na kutinga fainali ya Kombe la Ligi.
Griezmann ambaye alicheza sambamba na Lionel Messi katika kikosi cha FC Barcelona anavutiwa kwa muda mrefu na michezo na utamaduni wa Marekani na hajaweka siri ya kutaka kufurahia maisha ya MLS katika siku zijazo.
“Ndio, namfuata Messi,” alisema Griezmann akiwaambia waandishi wa habari.
“Leo ndiye bora katika historia, anajaza viwanja, anafunga mabao mengi na anashinda michezo.
“Yeye ni mzuri na nadhani ni jambo bora zaidi ambalo MLS wamefanya kumchukua Messi, katika suala la uuzaji na mpira wa miguu.” “Siku zote nimesema,”
“Lengo langu ni kuishia hapo, na kila kitu ninachopenda kuhusu michezo ya Marekani, kucheza kwenye MLS na kufurahia, kuweza kushinda vitu na kuwa katika kiwango changu bora.
“Kwanza nataka kuweka historia hapa na kushinda mataji pale Atletico. Baada ya hapo tutaona, nadhani uwepo Leo, Sergio Busquets na Jordi Alba ni mzuri kwa ligi. Hilo na kusajili wachezaji wachanga, hasa kutoka Amerika Kusini, ni jambo bora zaidi ligi inaweza lkufanya.” alisema Griezmann.
Mchezaji huyo alisema bado anatumaini kuweka historia huko Atletico lakini yuko wazi kuhusu kutaka kujaribu bahati yake nchini Marekani.
Griezmann mwenye umri wa miaka 32, alikuwa mmoja wa wachezaji bora wa La Liga msimu uliopita, akifunga mabao 15 na kutoa pasi za mabao 16 kwenye ligi huku Atletico Madrid wakimaliza nafasi ya tatu nyuma ya FC Barcelona na Real Madrid.