Meneja wa klabu bingwa nchini England (Chelsea FC) Antonio Conte amesema itamlazimu kutumia nguvu na ujuzi wa ziada ili kuhakikisha kikosi chake kinaibuka na ushindi katika mchezo wa mwishoni mwa juma hili dhidi ya Manchester United.

Conte amesema mchezo huo una umuhimu mkubwa sana kwa kikosi chake, hivyo hana njia ya mkato zaidi ya kuhakikisha anatumia njia mbadala za kuhakikisha lengo la kupata point tatu linatimizwa ipasavyo.

“Tunakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Manchester United na tunapaswa kushinda kwa nguvu na juhudi zetu zote, hatuna budi kufanya hivyo kama tunahitaji kuendelea kuwa kwenye njia ya kutetea taji la EPL,”

“Tunapaswa kufanya kazi kwa pamoja na kuelewa nini kinachotukabili mbele yetu, ninaamini kama tutakua hivyo hakuna kitakachotushinda kwenye mchezo huo.” Amesema Conte.

Chelsea kwa sasa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ya nchini England, na meneja huyo kutoka nchini Italia anaamini kama kikosi chake kitashindwa kuibuka na ushindi, huenda mipango ya kutetea taji lao ikashindwa kutimizwa ipasavyo mwishoni mwa msimu huu.

Chelsea kwa sasa wapo nyuma kwa pointi tisa dhidi ya vinara wa msimamo wa ligi hiyo Manchester City, na wanazidiwa pointi nne na wapinznai wao wa mwishoni mwa juma hili Manchester United wanaoshika nafasi ya pili.

Chelsea wameanza maandalizi ya kujiwinda na mchezo dhidi ya Manchester Unites, wakitokea nchini Italia walipopoteza mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya AS Roma kwa mabao matatu kwa sifuri, hali ambayo imewafanya washuke katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi la michuano hiyo.

Kipigo cha mchezo huo, kimeifanya Chelsea kupoteza jumla ya michezo mitatu tangu walipoanza msimu huu.

Chelsea haijawahi kufungwa na Manchester United kwenye uwanja wa Stamford Bridge tangu mwaka 2012.

Umoja wa Ulaya waineemesha Tanzania
Omog apania kuvunja rekodi uwanja wa Sokoine