Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Italia, Antonio Conte hii leo anatarajiwa kutangaza mustakabali wa kuendelea kuifundisha timu hiyo, ama kuondoka, kufuatia tetesi za kuhitajika kwenye klabu ya Chelsea yenye mskani yake makuu jijini London nchini England.

Conte, anatarajiwa kutangaza taarifa za mustakabali wake ili suala la kuwepo na kikosi cha The Azzurri lifahamike mapema kabla, hakijaelekea kwenye fainali za mataifa ya bara la Ulaya za mwaka huu (EURO 2016), ambazo zitaunguruma nchini Ufaransa mwezi Juni.

Taarifa zilizoripotiwa na kituo cha televisheni cha Rai Sport, zilieleza kwamba, kocha huyo ambaye aliwahi kukinoa kikosi cha Juventus, alitarajiwa kutangaza suala lake leo mchana lakini mpaka sasa bado hajafanya hivyo.

Msukumo mkubwa wa kufanya jambo hilo, umetolewa kwa Conte na baadhi ya maafisa wa shirikisho la soka nchini Italia, FIGC ambao wamekua wakikerwa na taarifa za kuondoka kwake ambazo hutolewa kila kukicha na vyombo vya habari vya England.

Conte, mwenye umri wa miaka 46, ana mkataba wa kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Italia hadi mwezi July mwaka huu, na jukumu zito lililo mbele yake ni kuhakikisha The Azzurri wanafanya vyema katika fainali za Ulaya(EURO 2016).

Hata hivyo taarifa nyingine zinadai kwamba uongozi wa klabu ya Chelsea, tayari umeshafikia makubaliano na shirikisho la soka nchini Italia, ili kuweza kumruhusu kocha huyo kuelekea jijini London kufanya kazi yake kama meneja mkuu wa The Blues.

Suala ni kusubiri na kuona kama harakati za Chelsea kumtwaa Antonio Conte zitafanikiwa ama kugonga mwamba, huku wataliano wengi wakimtaka mkuu huyo wa benchi la ufundi la timu yao ya taifa, aendelee kusalia mpaka mkataba wake utakapofikia kikomo.

Chelsea, walianza purukushani za kumsaka meneja, baada ya kumtimua kazi Jose Mourinho mwishoni mwa mwaka jana, kufuatia matokeo mabovu yaliyokua yakiwaandama katika michuano ya ligi ya nchini England.

Mkutano Mkuu Wa TFF Wamtunuku Heshima Leodger Tenga
Azam FC: Tutapambana Hadi Dakika Ya Mwisho Vs Bidvest