Mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Croatia na klabu ya Inter Milan Ivan Perisic amekuwa miongoni mwa wachezaji ambao wanatajwa huenda wakacheza soka nchini England msimu ujao wa 2016-17.

Perisic anapewa nafasi kubwa ya kuondoka nchini Italia, kufuatia kumvutia meneja mpya wa klabu ya Chelsea, Antonio Conte ambaye amekabidhiwa jukumu la kukifumua kikosi cha The Blues na kukisuka upya.

Kwa mujibu wa taarifa zinazochapishwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Italia, zinadai kwamba Conte ambaye mwanzoni mwa juma hili alisaini mkataba wa miaka mitatu na klabu ya Chelsea, amepanga kufanya usajili wa wachezaji watano wanaocheza ligi ya nchini Italia, ambapo miongoni mwa wahusika Perisic ni mmoja wapo.

Wengine wanaotajwa katika orodha ya Conte ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha timu ya taifa ya Italia kabla ya kuachia ngazi mara baada ya fainali za mataifa ya barani Ulaya mwaka 2016 (Euro 2016), ni Paul Pogba, Gonzalo Higuain  pamoja na Radja Nainggolan.

Wakala wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, Toni Martic, amesema tayari ameshakutana na viongozi wa klabu ya Inter Milan mara kadhaa kwa lengo la kuushurutisha ili wamuachie mwishoni mwa msimu huu endapo ofa ya klabu ya Chelsea itatua San Siro.

Amesema amefanya hivyo kutokana na Perisic kuwa na ndoto za kuhitaji kucheza katika ligi ya nchini England, hivyo anaamini ni wakati mzuri kwa mchezaji wake kwenda kutimiza ndoto zilizokua zikimkabili kwa muda mrefu.

‘Ni bahati ilioje kwa Perisic kutajwa kuwa sehemu ya wachezaji ambao watakwenda kucheza ligi ya nchini England, naamini ni muda mzuri kwake kuuthibitisha umma wa mashabiki duniani ni vipi anavyoweza kupambana akiwa uwanjani,’ Amesema Martic.

‘Ligi ya soka nchini England ni ligi kubwa na yenye umaarufu, tena inayofuatiliwa na watu wengi kila juma, naamini kama mambo yatakaa sawa Perisic atacheza Chelsea chini ya Antonio Conte.’ Ameongeza Martic.

Perisic alisajiliwa na Inter Milan mwaka 2015 akitokea nchini Ujerumani alipokua akiitumikia klabu ya VfL Wolfsburg na mpaka sasa ameshaichezea The Nerazzurri michezo 28 na amefunga mabao 6.

Pasi alizopiga na kumfikia mlengwa zina uwiyano wa asilimia 38, amepiga pasi zilizozaa magoli 23, pasi nyoofu asilimia 77 huku akionyeshwa kadi mbili za njano.

Purukushani Za Man Utd Kumpa Ulaji Mauricio Pochettino
Galliani: Sidhani Kama Tutaendelea Na Balotelli