Meneja wa klabu ya Chelsea Antonio Conte amesitisha mpango wa kuuzwa kwa kiungo wake kutoka nchini Serbia Nemanja Matic, ambaye anawaniwa na mabingwa wa Europa League Man Utd.
Conte amefikia maamuzi ya kusitisha mpango huo, kwa kuhofia huenda akashindwa kumpata mbadala wa Matic katika kipindi muafaka, hivyo ameona kuna haja ya kusubiri na kuona kama ataweza kuwahi kumsajili kiungo wa mabingwa wa Ufaransa AS Monaco Tiemoue Bakayoko.
Chelsea tayari wameshaonyesha nia ya dhati ya kumsajili kiungo huyo kutoka kutoka nchini Ufaransa, lakini wamekua wakikutana na vikwazo kutoka kwa viongozi wa AS Monaco.
Hata hivyo Antonio Conte ameelekeza macho yake kwa kiungo kutoka nchini Ubelgiji na klabu ya AS Roma ya Italia Radja Nainggolan, endapo itatokea anashindwa kumpata Bakayoko.
Matic amekua katika mipango ya meneja wa Man Utd Jose Mourinho katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi, na meneja huyo kutoka nchini Ureno amedhamiria kumsajili ili kuiboresha safu yake ya kiungo kwa ajili ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Mourinho anauhusudu uchezaji wa Matic tangu alipokua mkuu wa benchi la Ufundi la Chelsea, hali ambayo ilimpa msukumo wa kutaka kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 kusajiliwa tena Stamford Bridge, baada ya kuuzwa nchini Ureno katika klabu ya SL Benfica mwaka 2011.
Mwaka 2014 wakati Mourinho aliporejea Chelsea alifanikisha mpango huo, na kumtumia tena Matic katika kikosi cha The Blues.