Meneja wa klabu ya Chelsea Antonio Conte amesema hana shaka na mshambuliaji wa klabu hiyo Diego Costa, ambaye aliingia kwenye mzozo na benchi la ufundi la The Blues juma moja lililopita.
Conte alizungumza na waandishi wa habari kuhusu mshambuliaji huyo, mara baada ya mchezo wa jana wa ligi kuu ya soka nchini England, ambapo Chelsea walicheza nyumbani dhidi ya Hull City.
Mshambuliaji huyo alifunga bao la kwanza katika dakika ya 45 ya mchezo huo, kabla ya beki Gary Cahill hajaongeza la pili katika dakika ya 81.
Conte, alisema hatua ya kurejea uwanjani kwa mshambuliaji huyo na kufunga bao, inadhihirisha ni mwenye furaha na amemaliza minong’ono iliyokua ikiendelea kupitia vyombo vya habari.
Alisema siku zote amekua akifurwahishwa na uwezo wa mshambuliaji huyo mzaliwa wa nchini Brazil, na alitambua Costa atakaporejea uwanjani ataweza kucheza soka na kuendelea kufunga.
Costa ambaye ni raia wa nchini Hispania, amefikisha mabao 52 tangu alipojiunga na klabu ya Chelsea mwaka 2014 akitokea Atlético Madrid, huku akicheza michezo 100.
Wakati wa mchezo dhidi ya Leicester City, Costa aliachwa nje ya kikosi, kwa kigezo cha kuwa majeruhi, lakini taarifa za vyombo vya habari zilieleza, alikua na tofauti na Antonio Conte.