Meneja wa klabu ya Chelsea Antonio Conte, amekiri kuwa katika wakati mgumu wa kutimiza jukumu la usajili wa wachezaji aliowakusudia katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

Conte ambaye alikabidhiwa kikosi cha Chelsea kutoka mikononi mwa aliyekua meneja wa muda huko Stamford Bridge msimu uliopita Guus Hiddink, amesema kumekua na changamoto kubwa katika mipango ya usajili aliyojiwekea kutokana na ushindani uliopo sokoni.

Amesema jambo hilo limekua likimpeleka puta na kuamini atakua na shughuli nzito ya kukamilisha malengo aliyojiweka katika usajili wa wachezaji aliowakusudia, ili kukamilisha mikakati ya kuirejesha mahala pazuri Chelsea ambayo ilishindwa kufurukuta msimu uliopita katika ligi ya nchini England.

“Msimu huu hali imebadilika sana katika suala la usajili, pamekua na ushindani mkubwa, na wachezaji wamekua na gharama kubwa,”

“Kila mchezaji unaemlenga kwa ajili ya kumjumuisha kikosini mwako, ana changamoto zake na wakati mwingine ukiangalia pesa ulionayo haitoshi hivyo inakulazimu kusaka mbinu mbadala ili ufanikishe suala la kumsajili. Japo natambua hali itaendelea kuwa ngumu zaidi hadi dirisha litakapofungwa mwishoni mwa mwezi ujao.”

“Wakati mwingine unaweza ukajikuta unatumia kiasi kikubwa cha pesa tofauti na bajeti iliyokusudiwa, inaweza ikawa Pauni milion 100, 120 au hata 95, ila hakuna njia ya mkato zaidi ya kupambana katika suala la ushindani uliopo.” Alisema Conte alipozungumza na waandishi wa habari mjini California nchini Marekani ambapo kikosi chake kimeweka kambi.

Tayari Chelsea wameshatumia kiasi cha Pauni milioni 64 kwa usajili wa wachezjai wawili ambao ni  Michy Batshuayi na N’Golo Kante na bado wapo katika mawindo ya kuwasaka Alvaro Morata, Romelu Lukaku na Kalidou Koulibaly.

Valencia CF Yamuweka Sokoni Shkodran Mustafi
West Ham Utd Wakaribia Kunasa Kinda La Argentina