Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) na taasisi zilizo chini ya sekta hiyo zipo katika utekelezaji wa mpango mkakati shirikishi wa kukamilisha mpango wa anwani za makazi na postikodi unaotarajiwa kufikia halmashauri zote nchini ifikapo mwaka 2022 ili kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kidigitali.
Akizungumza katika ziara ya kukagua uwekaji wa namba za nyumba katika kata Tatu za Chamwino Ikulu, Ipagala na Hazina, jijini Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa ukamilishaji wa mpango huo utarahisisha shughuli za biashara mtandaoni na huduma za posta mlangoni.
“Wizara ipo kwenye utekelezaji wa mkakati wa kuhakikisha kila nyumba inakuwa na anwani ya makazi inayojumuisha jina la barabara, mtaa na namba ya nyumba, ili wananchi waweze kufikiwa katika maeneo wanayoishi kwa urahisi na kukuza biashara mtandao na posta mlangoni kuelekea uchumi wa kidijitali”, amezungumza Dkt. Chaula.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara hiyo, Mhandisi Clarence Ichwekeleza amesema kuwa, mpango wa anwani za makazi na postikodi unatambulika kimataifa na ukamilishwaji wake utasaidia kuongeza fursa za kibiashara na kujiajiri hasa kwa upande wa biashara mtandao ambapo wananchi wataweza kuagiza bidhaa na kuletewa mpaka mlangoni.
Utekelezaji wa zoezi hilo unahusisha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,TAMISEMI, Halmashauri na wadau mbalimbali ambapo kazi inayoendelea kwa sasa ni uwekaji wa namba za nyumba katika halmashauri za jiji la Dodoma chini ya mkandarasi SUMA JKT ambapo jumla ya nyumba 21,947 zitawekewa namba kati ya nyumba 30,152.
Mpango wa uwekaji wa anwani za makazi na postikodi umetekelezwa katika kata 116 nchini kati ya kata 3956, kwenye Halmashauri 18 kati ya 185 nchini.