Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Nchini Kenya, Kenyatta Hospital, Lilly Koros amepewa likizo ya lazima mara baada ya mgonjwa kufanyiwa upasuaji wa ubongo kimakosa katika hospitali hiyo.
Hatua hiyo ya kumpeleka likizo ya lazima kiongozi huyo imetangazwa na Waziri wa afya, Sicily Kariuki ambaye amesema hatua hiyo inakusudiwa kupisha uchunguzi.
Tukio hilo ambalo limewashangaza wengi lilitokea katika hospitali hiyo wiki iliyopita na leo ilikuwa tarehe ya mwisho kwa maafisa wa matibabu ambao walihusika kueleza ilikuwaje hadi kosa hilo likatokea.
Katika taarifa iliyotolewa na Bi Koros imesema kuwa kosa hilo lilitokea pale mkanganyiko ulipotokea kuhusu wagonjwa wawili waliokuwa hawajitambui.
Hata hivyo, Bi Koros ameomba radhi na kusema anafuraha kubwa kuwatangazia umma kwamba mgonjwa huyo sasa ametibiwa na anaenedelea vizuri.