Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 17, amekimbizwa katika hospitali ya Tennessee Marekani wiki hii baada ya kupigwa risasi na rafiki yake katika harakati za kuigiza video kwa ajili ya kuweka Facebook kufuatia shindano maarufu linaloendelea kwenye mtandao huo.
Katika mtandao huo wa kijamii, kuna shindano linaloitwa ‘no lackin challenge’, ambao watu hujirekodi wakifanya jaribio la kuoneshana bastola kwa njia mbalimbali, lakini hauruhusiwi kufyatua risasi hata kama ni feki. Kwa kawaida wengi hutumia bastola feki.
Kijana mwenye umri wa miaka 21, Sherman Lackland amejikuta mikononi mwa polisi baada ya kufyatua risasi bahati mbaya katika harakati za kujirekodi iliyompata rafiki yake huyo.
Shuhuda wa tukio hilo, Thomas Fitzpatrick ameiambia Daily Mail kuwa vijana hao walikuwa wamekaa muda mrefu sehemu moja, na baadaye aliona mmoja wao akatoa bastola na kumuelekezea mwenzake wakitaniana, kabla ya kusikia mlio mkubwa wa risasi.
“Aliyefyatua risasi hiyo nilimuona anahangaika kumuamsha rafiki yake akitapatapa kama amechanganyikiwa hivi. Kwa bahati nzuri kulikuwa na baadhi ya madaktari waliokuwa wanakula kwenye mgahawa mmoja karibu na eneo hilo, ndio waliomsaidia kutoa huduma ya kwanza kuokoa maisha,” alisema Fitzpatrick.
- Aliyemmwagia mwanaye tindikali aachiwa, Mahakama yaridhia sababu
- Rick Ross awatuliza mashabiki wa Diamond
Kumekuwa na mashindano mengi ya hatari yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na shindano la kula pilipili kali au kavukavu au barafu na chumvi.