Mchezaji wa mchezo wa kugonga kwenye barafu (Curling), Alexander Krushelnitsky wa Urusi amepokonywa medali yake ya shaba aliyoipata hivi karibuni katika Olimpiki ya majira ya baridi inayoendelea mjini Pyeongchang nchini Korea Kusini baada ya kukiri kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni.
Siku chache zilizopita vipimo vilimuonesha mchezaji huyo kuwa alitumia dawa aina ya meldonium lakini alikana kuhusika na tuhuma hizo kwa madai kuwa aliwekewa mtego kwenye kinywaji chake kabla ya mapema hii leo kuamua kuondoka rufaa yake huku akikiri kuwa kweli alitumia dawa hiyo.
Kufuatia kosa hilo, mchezaji huyo huyo amefungiwa kwa kipindi chote cha mashindano huku medali ya shaba aliyoshinda yeye na mkewe ikitunukiwa kwa wanariadha wa Norway walioshika nafasi ya nne.
Alexander mwenye umri wa miaka 25 ni miongoni mwa wanamichezo 168 wa Taifa la Urusi walioruhusiwa kushiriki mashindano hayo kwa kivuli cha kuwa wanamichezo huru.