Klabu ya APR FC ya Rwanda ipo kwenye mipango ya kuwasilisha ofa kwa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa usajili wa Mshambuliaji Meddie Kagere.
APR wanatajwa kuwa kwenye mpango huo ili kujiweka sawa katika eneo la ushambuliaji kuelekea kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu ya Rwanda.
Kagere amekua na wakati mgumu wa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza tangu kocha Gomes alipowasili Msimbazi mwanzoni mwa msimu huu.
Hata hivyo licha ya kupata changamoto hizo, bado Mshambuliaji huyo kutoka Rwanda amejipapatua na kumaliza katika nafasi ya nne kwenye orodha ya wafungaji Bora, kwa kufunga mabao 13.
Huenda juhudi za Mshambuliaji huyo aliejiunga na Simba SC mwaka 2018 akitokea Gor Mahia ya Kenya, zimewavutia APR na wanaamini bado ana kitu kitakachowasaidia.
Endapo APR itafanikiwa kumsajili nyota huyo, Kagere atakuwa ameungana na swahiba wake Jacques Tuyisenge ambaye aliwahi kucheza nae Gor Mahia kwa kiwango kikubwa.
Bado klabu ya Simba SC na Kagere hawajazungumza lolote kuhusu tetesi hizo, lakini huenda wakafunguka endapo APR watatuma ofa huko Msimbazi.