Klabu ya Young Africans imesema haina shaka na mechi ya Ligi ya Mabingwa itakayochezwa Jumamosi ijayo dhidi ya Al Merrikh ya Sudan kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam ikitamba kuwa itamalizia ilipoishia.
Makamu wa Rais wa Klabu hiyo, Arafat Haji, amesema ushindi wa mabao 2-0 ugenini katika Uwanja wa Kigali Pele, nchini Rwanda, uliochezwa Septemba 16, mwaka huu, unawapa matumaini makubwa ya kutinga hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu 1998.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Arafat amesema kingine ni ubora wa Kocha wao Mkuu, Miguel Gamondi na kikosi chao pia unawapa jeuri ya kutimiza malengo yao ya awali ya kutinga hatua hiyo.
“Tunajua mchezo haujamalizika, dakika 90 za mchezo wa kwanza zimekwisha pale Kigali, Rwanda na Mungu akatujaalia tukapata ushindi wa mabao 2-0 ugenini, lakini kwa kuiangalia timu yetu, maandalizi ya mwalimu Miguel Gamondi, na ubora wa kikosi chetu, basi ni matumaini yetu kuwa tunakwenda kukamilisha pale palipobakia na kusonga hatua inayofuata ya makundi,” amesema kiongozi huyo.
Amesema watakapofanikiwa kutinga hatua hiyo, hatua inayofuata itakuwa ni kujipanga wao kama Uongozi na kuangalia jinsi gani watavyocheza hatua hiyo na lengo lao litakuwa kufika mbali.
“Kwa awamu hii ya kwanza hatua yetu ni kufuzu kutinga makundi na tukishafika huko tutajipanga ili kuona tunafika mbali kwenye michuano hiyo baada ya hapo, niwasihi tu wanachama na mashabiki wa Young Africans kujitokea kwa wingi kuwapa morali wachezaji wetu kuhakikisha wanakamilisha ile kazi ambayo tumewatuma, kama tulikuwa wengi kule Kigali, Rwanda besi tunaoneshe kuwa hapa ni nyumbani, amesema Arafat.
Yanga ina matumaini makubwa ya kutinga makundi kutokana na kumiliki kwa kiasi kikubwa mechi ya kwanza nchini Rwanda, huku wapinzani wao wakionekana kupaki basi zaidi kuliko kushambulia.
Al-Merrikh ilicheza nchini Rwanda badala ya Sudan kutokana machafuko makubwa ya kisiasa nchini mwao ambapo kwa kiasi kikubwa imeziathiri timu za nchini humo kwani zime kuwa dhaifu kutokana na kutowapo kwa ligi, lakini pia wachezaji wao wengi wa kigeni kuamua kuondoka kwa kuvunja mikataba yao.
Young Africans ambayo msimu uliopita ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, inahitaji ushindi wowote katika mechi hiyo ya Jumamosi, sare yoyote au isifungwe mabao yanayoanzia mawill ili kutinga makundi kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24 kupita.