Makamu wa Rais wa Young Africans, Arafat Haji, ameibuka na kutamka kuwa, sasa hivi wanataka kuona inakuwa kawaida kwa timu yao kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kauli yake imekuja baada ya Young Africans kuweka historia msimu huu ya kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kupita miaka 25.
Wakati Young Africans ikitinga hatua hiyo, zipo baadhi ya klabu kubwa ambazo zenyewe kawaida kwao kufika hatua hiyo, kati ya hizo ni Al Ahly, Esperance, Pyramids, Raja Casablanca, Wydady Casablanca, RS Berkane, Simba SC, Mamelod Sundowns na Orlando Pirates.
Arafat amesema kuwa uongozi umeandaa mikakati mikubwa ya kuhakikisha kila msimu wanafuzu kuanzia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hilo linawezekana kutokana na malengo waliyoweka viongozi.
Arafat amesema kuwa wanataka kuona mashabiki wao wanazoea na kuona kawaida, timu yao ikifuzu makundi ya michuano hiyo, baada ya kuteseka kwa miaka 25.
Ameongeza kwa kuwapongeza wachezaji wao kucheza kwa kujitoa, na kufanikiwa kufikia malengo yao ya kwanza katika msimu huu ambayo ni kufuzu hatua ya makundi.
“Ninashukuru kuwa mmoja wa viongozi waliofanikisha historia katika msimu huu, ambayo ni kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 25, sio kitu kidogo nikiwa kama Makamu wa Rais wa Young Africans.
“Kama uongozi tumejipanga tuwe na mwendelezo mzuri wa kufika kuanzia Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa kuanzia msimu huu na kuendelea mbele.
“Kikubwa tunataka kuona Young Africans inakuwa kawaida kufuzu makundi, hivyo tutahakikisha tunafanya usajili mkubwa wa wachezaji bora katika ukanda huu wa Afrika, ili tufikie malengo yetu hayo,” amesema Arafat.