Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ limethibitisha nchi ya  Argentina itakuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 20.

Awali Fainali hizo zilipangwa kufanyika nchini Indonesia kabla ya kupokwa haki hiyo mwezi uliopita.

FIFA ilitangaza uamuzi wa kuipoka Indonesia uenyeji huo Machi 29 baada ya Shirikisho la Soka la nchi hiyo kuahirisha Droo iliyopangwa kufanyika Bali baada ya Gavana wake kukataa kuikaribisha timu ya Israel.

Shirikisho la Soka la Argentina ‘AFA’ liliwasilisha ombi lake la kuandaa michuano hiyo itakayofanyika Mei 20-Juni 11 mwaka huu 2023, siku moja baada ya kumalizika kwa mkutano wa Shirikisho hilo kutoka Amerika ya Kusini.

“Napenda kuishukuru AFA, Rais wake Claudio Tapia na mamlaka za serikali kwa kukubali kuandaa Fainali hizo, licha ya kupata taarifa kwa kuchelewa,” amesema Rais wa Fifa, Gianni Infantino.

“Kwa vile michuano ya mwaka huu itafanyika kwenye nchi ambayo soka inaishi, bila shaka itafana na tutapata nyota wa baadae.”

FIFA imesema sasa Droo ya Fainali hizo itafanyika keshokutwa mjini Zurich.

Argentina iliandaa Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 mwaka 2001 na wakashinda taji la nne kati ya sita waliyonayo.

Nchi hiyo ndio mwandaaji wa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2030 kwa ushirikiano na Uruguay, Chile na Paraguay.

Lionel Messi aliiongoza nchi hiyo kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya tatu kwa timu yao ya wakubwa nchini Qatar, Desemba mwaka 2022.

Wakongwe wampongeza Gabriel Geay
Wabunge wa Mbeya waibeba Mbeya City Ligi Kuu