Mabingwa wa soka barani Afrika, timu ya taifa ya Cameroon wanatajwa kuwa timu pekee itakayoshiriki fainali za kombe la Mabara za mwaka huu huko nchini Urusi, huku wakiwa na msukumo wa kumbukumbu ya aliyekua kiungo wa timu hiyo Marc Vivien-Foe.
Foe alifikwa na umauti wakati wa fainali za kombe la mabara za mwaka 2003, zilizounguruma nchini Ufaransa, ambapo kiungo huyo alianguka mwenyewe eneo la katikati ya uwanja katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Colombia.
Akiwa na umri wa miaka 28 wakati huo, Foe alikua anatazamwa kama mkombozi wa taifa la Cameroon ambalo liliingia fainali na kucheza na Ufaransa.
Fainali za kombe la mabara zinazoanza rasmi leo huko nchini Urusi, zitakua zinakumbusha miaka 14 ya kifo cha Foe ambaye alikua akiitumikia klabu ya Man City ya England.
Cameroon wataanza kampeni za kuwania ubingwa wa mabara kwa kucheza na mabingwa wa Amerika ya kusini, timu ya taifa ya Chile katika mchezo wa kundi B siku ya jumapili (Kesho) mjini Moscow, kisha watawavaa mabingwa wa barani Asia Australia siku nne baadae, na watamaliza michezo ya makundi kwa kupambana na mabingwa wa dunia, timu ya taifa ya Ujerumani, Juni 25.
Kiungo wa timu ya taifa ya Cameroon Arnaud Djoum, amezungumza na shirika la utangazaji la Uingereza BBC na kueleza namna watakavyo pambana vilivyo ili kuenzi mchango wa Marc Vivien-Foe.
Djoum, amesema lengo lao ni kutaka kuonyesha bado wanamkumbuka Foe kwa matendo yake ya kizalendo, ambayo wakati wote yalionekana uwanjani na kuishia uwanjani.
Mpaka anafikwa na umauti Marc Vivien-Foe, alikua ameshaitumikia timu ya taifa ya Cameroon katika michezo 62 na kufunga mabao manane.