Meneja wa wa Arsenal, Arsene Wenger anaamini timu hiyo itajichanganya msimu ujao, endapo aitashindwa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Arsenal imepewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa msimu huu hata hivyo imejitibulia katika mechi nne za mwisho ilizocheza.
Ikumbukwe ilikuwa kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya pointi nane dhidi ya Manchester City, lakini baada ya kushinda mchezo mmoja katika mechi tano za mwisho ikaangua pua.
Sasa Man City ndio inapewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa wa ligi baada ya kuiondoa Arsenal kileleni kwenye msimamo wa ligi, huku Wenger akisisitiza imechezea nafasi vibaya.
Wenger amemsifia Mikel Arteta kutokana na kazi kubwa ya kujenga kikosi cha Arsenal na anaamini itakuwa timu ya ushindani miaka ijayo.
Wenger alitoa kauli hiyo katika tuzo za ugawaji wa ‘Hall of Fame’ kwa wachezaji wakongwe ambao waliwahi kufanya mambo makubwa kwenye Ligi Kuu England.
Wakongwe hao waliotambulika na kupewa tuzo maalumu ni Tony Adams, Rio Ferdinand, Petr Cech pamoja na kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson.
Mfaransa huyo alishinda mataji matatu ya ligi alipokuwa Arsenal, lakini kikosi hicho chenye maskani yake jijini London hakijabeba ubingwa tangu 2004.
Man City ipo kileleni mwa ligi kwa alama 79 tofauti ya alama moja dhidi ya Arsenal inayoshika nafasi ya pili.