Klabu ya Arsenal imepanga kumjumuisha kiungo kutoka nchini Ufaransa Matteo Guendouzi kwenye ofa ya kumsajili kiungo mshambuliaji kutoka Brazil na FC Barcelona Philippe Coutinho.
Coutinho ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo kwa mabingwa wa Ujerumani FC Bayern Munich amekuwa akihusishwa na harakati za kutaka kurejea tena England baada ya kutoonyesha kiwango kilichotegemewa ndani ya FC Barcelona na alisajiliwa dirisha dogo mwaka 2018.
Hata hivyo, Arsenal hawako pekee yao kwenye mkakati wa kuhitaji huduma ya Coutinho, pia Chelsea, Tottenham, Leicester City na Newcastle United zimeonyesha nia ya kumuhitaji kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28.
Arsenal inataka kumuunganisha Guendouzi katika dili hilo kwa kuwa Kocha Mikel Arteta ameweka wazi hamhitaji ndani ya kikosi chake kwa msimu ujao, kutokana na vitendo vyake vya kuonyesha nidhamu mbovu.
Pia inadaiwa washika mitutu hao wanafikiria kuwatoa wachezaji wawili ili kufanya mabadilishano bila ya kutumia pesa kwenye dili hilo.
Inadaiwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Arsenal, Edu amekuwa anamfatilia kwa muda mrefu Coutinho huku mabosi wa Barcelona pia wakiripotiwa kuwa na mpango wa kumsainisha Guendouzi kwa muda mrefu, jambo linalosababisha dili hilo kuwa na zaidi ya asilimia 70 za kukamilika.
Barcelona ina mkataba na mchezaji huyo hadi mwaka 2023, huku bei yake kamili ikiwa ni Pauni 60 milioni, lakini baadhi ya vyombo vya habari kutoka nchini Hispania zinadai mchezaji huyo huenda akasalia Barca ili kupigania namba yake kwa msimu ujao.