Mkuu wa kitengo cha soka cha klabu ya Arsenal Raul Sanllehi, amesema huenda wakaingia sokoni mwezi Januari wakati wa dirisha dogo la usajili, kufuatia kuumia kwa mshambuliaji Danny Welbeck ambaye itamchukua muda mrefu kurejea tena dimbani.
Welbeck, ambaye aliumia goti na kifundo cha mguu majuma mawili yaliyopita akiwa katika mchezo wa Europa League dhidi ya Sporting Lisbon, hatoweza kucheza soka hadi msimu ujao wa ligi, hali ambayo inamfanya meneja wa Arsenal Unai Emery, kufikiria namna ya kuziba pengo lake.
Sanllehi amesema wakati wakifikiria kuingia sokoni mwezi Januari 2019, kuna uwezekano mkubwa wa mshambuliaji kinda Eddie Nketiah kuchukua nafasi ya Welbeck katika kipindi hiki cha kuelekea dirisha dogo la usajili.
“Huo ndio mpango wetu, tunafikiria kufanya usajili wa mshambuliaji mwezi Januari, ” alisema Sanllehí alipohojiwa na gazeti la The Independent la England.
“Sina uhakika sana ni nani atawekwa katika rada za meneja Unai Emery, lakini kuna ulazima wa kuingia sokoni kutafuta mshambuliaji ambaye atakua na uwezo mkubwa wa kupambana, japo katika kipindi hiki meneja anafikiria kumtumia kijana Eddie Nketiah.”
Welbeck ambaye alisajiliwa klabuni hapo mwaka 2014 akitokea Manchester United, tayari ameshaitumikia Arsenal katika mchezo 88 na kufunga mabao 16.