Klabu ya Arsenal na Manchester City zimeingia mwezi huu wa Aprili zikikabiliwa na vita kali katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England wakati zikiwa zimebaki mechi chache za kumalizia msimu.
Arsenal imeketi kileleni kwa tofauti ya alama nane baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Leeds United, wakiwajibu Man City waliowachapa 4-1 Liverpool mwishoni mwa juma lililopita.
Lakini, Man City ya Pep Guardiola bado ina mchezo mmoja mkononi na hapohapo kuna mchezo mmmoja watakipiga na Arsenal mwishoni mwa mwezi huu.
Man City wanaamini watawakamata Arsenal kwenye mbio hizo, ambao wao wanasaka taji lao la kwanza la ligi baada ya miaka 19. Kuna uwezekano wa timu hizo mbili kukutana kwenye mchezo wa mchujo kuamua bingwa.
Utaratibu wa Ligi Kuu England, ubingwa unaamuliwa na alama na kama alama zimelingana basi ni tofauti ya mabao, kisha mabao ya kufunga.
Tofauti ya mabao, Man City ipo juu kwa mabao mawili na upande wa mabao ya kufunga, chama hilo la Guardiola lipo mbele kwa bao moja.
Kama vitu vyote hivyo vitalingana hadi itakapofika mwisho wa msimu, yatatazamwa matokeo ya mchezo wenyewe kwa wenyewe walipokutana, kuona nani alishinda, kama kila mtu alishinda, nani alipata mabao mengi ugenini.
Kama kote kutafanana, basi utapigwa mchezo mmoja ya mchujo. Lakini, kwa sasa hivi Arsenal, itahitaji kupata ushindi wa mabao matatu itakapokwenda kukabiliana na Man City uwanjani Etihad.
Lakini, hilo la kufikia hatua hilo lije kutokea, basi chama hilo la Mikel Arteta litahitaji kupoteza pointi kiasi cha kuwafanya wafikiwe kileleni.
Walivyo Arsenal kwenye moto wao wa sasa hawaonekani kama watapoteza pointi kiasi cha kuwafanya hadi wafikiwe kileleni, wakati ligi imebaki mechi tisa na wapo juu kwa alama nane.