Meneja msaidizi namba mbili wa klabu ya Liverpool Zeljko Buvac, anatajwa kuwa miongoni mwa wanaowaniwa na klabu ya Arsenal ambayo kwa sasa inamsaka mrithi wa Arsene Wenger.
Buvac, ameomba ruhusa ya kushughulikia masuala ya kifamilia uongozi wa Liverpool hadi mwishoni mwa msimu huu, lakini tayari imeanza kuhisiwa huenda akawa anajiandaa kufanya mazungumzo na viongozi wa Arsenal, ambao wanaendelea na mchakato wa kumsaka bosi wa benchi lao la ufundi.
Meneja huyo raia wa Bosnia anaejulikana kwa jina la utani ‘The Brain’, ana uzoefu wa kukaa kwenye benchi la ufundi kama msaidizi Klopp kwa miaka 17, na walikua wote tangu wakiwa na klabu za Mainz na Borussia Dortmund zote za Ujerumani, kabla ya kujiunga na Liverpool.
Hata hivyo bado haijathibitishwa ni lini Buvac atakutana na viongozi wa Arsenal kufanya mazungumzo ya awali, lakini tayari imeanza kuripotiwa na vyombo vya habari vya England, juu ya uhakika wa kuchukua kiti cha Arsene Wenger.
Wakati Arsenal ikihusishwa na meneja huyo, mameneja wengine wanaotajwa kuwa katika mlolongo wa kurithi nafasi ya Arsene Wenger ni Massimiliano Allegri, Carlo Ancelotti, Luis Enrique, Brendan Rodgers, Eddie Howe, Mikel Arteta, Leonardo Jardim, Patrick Vieira pamoja na Joachim Loew.