Kocha Mkuu wa Washika Bunduki ya Kaskazini mwa jijini London, Mikel Arteta ameripotiwa kuwa kwenye mpango wa kuwasilisha ofa ya kumnunua Kiungo wa Kati kutoka nchini Brazil na Klabu ya Aston Villa Douglas Luiz Soares de Paulo, ikiwa ni mwaka mmoja tangu aliposhindwa kumsajili.
Mpaka sasa Arsenal tayari imekamilisha usajili wa mastaa watatu wa nguvu ambao ni Kai Havertz, Jurrien Timber na Declan Rice lakini inaelezwa watalazimika kuingia tena kwenye soko la usajili iwapo Thomas Partey ataondoka katika klabu hiyo.
Villa ilikataa ofa mbili kutoka kwa The Gunners kwa ajili ya Luiz, mwenye umri wa miaka 25, msimu uliopita wa joto ambapo mchezaji huyo alikuwa ameingia mwaka wa mwisho wa kandarasi yake na Mikel Arteta alituma dau la Pauni milioni 23 siku ya mwisho, ambalo lilikataliwa.
Villa wamemshawishi Luiz kusaini mkataba mpya wa muda mrefu, hata hivyo inaaminika Arsenal bado wana nia ya kumsajili nyota huyo wa zamani wa Manchester City na watafikiria kuzindua ofa mpya msimu huu wa joto.
The Gunners wanawinda kiungo mpya wa kati kutokana na hali ya Thomas Partey ambaye anawindwa vikali na Juventus na timu za nchini Saudi Arabia ambao wanaonyesha nia ya kumsajili mchezaji huyo wa kimataifa wa Ghana.
Inaaminika Arteta anataka Partey abaki, lakini kocha huyo wa Arsenal atalazimika kuingia kwenye soko la usajili iwapo ataondoka.
Kama ilivyoripotiwa na The Sun, The Gunners wanataka kumsajili Luiz msimu huu wa joto lakini wanakabiliwa na ushindani kutoka kwa wapinzani wao Tottenham.
Spurs ambao wako chini ya utawala mpya kufuatia kuwasili kwa Ange Postecoglou kutoka Celtic, mapema msimu huu wa joto na wanataka kujenga kikosi kitakachofuzu kwa katika Michuano ya Uropa.
Tayari wamewasajili James Maddison, Guglielmo Vicario na Manor Solomon.